Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos
Makala juzi aliwekwa kitimoto na baadhi ya wakulima wilayani Mvomero
mbele ya mawaziri wengine wanne katika mkutano ulioitishwa kutafuta
suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mkindo.
Makala ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero ulipo
mgogoro huo, alilalamikiwa na wakulima hao wakidai kwamba amekuwa
akiwasikiliza zaidi wafugaji na kutoonyesha jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo kwa
agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chizza, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Nchimbi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck
Ole-Medeye.
Akijibu shutuma zilizoelekezwa kwake, Makala
alisema: “Msiseme tu mwangalie na juhudi zangu. Namshukuru Dk Nchimbi
kwa kusoma barua ya Waziri Mkuu, uongo umejitenga na ukweli
umedhihirika. Mimi nikiwa mbunge ni mwakilishi wa wananchi, nimewaita
mawaziri hapa, nimekuwa kama mshenga ili wasikie malalamiko yenu,”
alisema Makala.
Malalamiko ya wananchi
Katika malalamiko yao, wakulima hao walisema licha
ya uonevu wanaoupata kutoka kwa wafugaji na Jeshi la Polisi, mbunge wao
amekuwa kimya.
“Mbunge wetu hatusaidii kitu kila tunapopata
matatizo. Yalipotokea machafuko Kijiji cha Hembeti hakuonekana. Kuna
taarifa zisizo rasmi kuwa amekuwa akifanya mapatano na wafugaji kwa
siri,” alisema mmoja wa wanakijiji wa Mkindo, Shomari Msumi na kuongeza:
“Watoto wetu wamelazwa Hospitali ya Bwagala,
Polisi wamekuja kuwafunga pingu na kuondoka nao, wafugaji hawaguswi kwa
sababu ya nguvu ya fedha. Vyombo vya Dola hasa Mahakama nayo
inatukwamisha. Mazao yameliwa lakini kesi haziamuliwi, hadi leo kesi iko
wilayani.”
Mkulima mwingine, Aziz Dendego alisema:
“Tunaumizwa mno na viongozi wa wilaya. Mimi nimefika hapa mwaka 1975.
Kero zimeanza miaka 20 iliyopita na Serikali ndiyo inayosababisha. Mkuu
wa Mkoa anaagiza tu lakini hatuoni vitendo. Mkuu wa wilaya alikuwa mzuri
lakini sasa amebadilika kabisa. Bunduki za kijeshi zimetumika kwenye
mapigano, wakulima wamezipataje?”
Mmoja wa wakulima hao, Shaaban Khamis alisema
wameamua kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi baada ya kulalamika kwa
muda mrefu bila kusikilizwa.
Wakulima hao pia wamemlalamikia Mwenyekiti wa
Kijiji cha Wafugaji cha Kambala waliyemtaja kwa jina moja la Kashu
wakidai kuwa amekuwa akiongoza mapigano dhidi ya wakulima.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Hata hivyo, Kashu hakuhudhuria mkutano huo ambao wafugaji waliwakilishwa na mfugaji mmoja tu, Majuka Koila.
“Watu wameuawa, nyumba 380 zimechomwa moto na
wafugaji katika Kijiji cha Kwa Mbogo, hadi leo hakuna aliyekamatwa,”
alisema Hassan Said.
Mawaziri wamtetea
Licha ya Dk Mathayo kuahidi kujenga majosho na
mabwawa ya kunyweshea mifugo, alimtetea Makala kuwa amekuwa akimsumbua
kuhusu matatizo ya wakulima.
“Makala anakaa nyuma yangu pale bungeni, amekuwa akinisumbua sana. Mbunge wenu anawapenda,” alisema na kuongeza:
“Lazima wafugaji wafuate sheria na utaratibu.
Matatizo haya yanatokana na ukosefu wa miundombinu hasa malambo na
majosho. Tutayajenga ili wafugaji wasiingie kwa wakulima.”
Huku akimtetea Makala, Naibu Waziri, Ole-Medeye alitaja mikakati mitatu ya Serikali.
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Shetani
kazi yake ni kusababisha vita na ugomvi kati ya ndugu na ndugu. Makala
amenisumbua sana. Migogoro mingi imekuwapo kabla hata hajaingia
madarakani. Kwa mfano, mgogoro huu wa Bonde la Mgongola umeanza mwaka
2005, Makala alikuwepo?”
Kuhusu utatuzi wa mgogoro huo, Ole Medeye alisema
amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumaliza suala hilo nje ya
mahakama ili kuleta suluhu.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka
alipojaribu kumtetea kwa kuwauliza wananchi kama Waziri Makala
ameshawatembelea mara ngapi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkindo, Ally
Shamte alisema amefika mara moja tu tangu achaguliwe.
Waziri Chizza alikiri kuwa kero za wakulima
zinatokana na kutopewa majibu haraka... “Lipo tatizo la kutotoa majibu
haraka. Tunao mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), tunapaswa kutoa
majibu sasa siyo kusubiri matukio. Tusingependa kuja hapa baada ya watu
kufa, maana hatuwezi kuwafufua,” alisema Chizza.
Makala ajitetea
Baada ya mawaziri hao kujieleza, Chizza alimpa nafasi Makala ambaye alieleza kwa kina jinsi alivyoshughulikia migogoro hiyo.
“Ulipotokea mgogoro wa Kijiji cha Lukenge, nilikaa
na wafugaji wa Kijiji cha wafugaji cha Sokoine na siku hiyohiyo nilikaa
na wakulima wa Kijiji cha Sigaju. Siku walipofunga barabara nilikuwa
mkoani Iringa kwenye sherehe za kuzima Mwenge. Watu wanafanya siasa,
wengine wananipigia simu na kuniuliza niko kijijini, hayo ni mambo ya
siasa tu,” alisema na kuongeza:
“Mgogoro wa Bonde la Mgongola tumekuja pale
wakatoa tamko, shamba la Kijiji cha Begi hakuna mwanasiasa yeyote
aliyeshughulikia zaidi yangu. Nimekaa pale hadi saa mbili usiku. Hata
wale vijana waliosingiziwa kesi nimetoa fedha yangu mfukoni kuwatoa.”
Dk Nchimbi awajia juu polisi
Licha ya kumtetea Makala, Dk Nchimbi alishangazwa
na Jeshi la Polisi mkoani humo kutowakamata wafugaji waliohusika katika
mapigano hayo.
“Binafsi sijaridhishwa na idadi ya wafugaji
waliokamatwa. Haiwezekani wauawe watu sita, wakulima wanne na wafugaji
wawili halafu wakamatwe wakulima 32 na wafugaji wawili. Hakikisha
unafanya operesheni ya kuwakamata waliohusika,” alisema Dk Nchimbi.
Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile alikanusha kuwa bunduki zilizotumika kwenye mapigano
hayo zilikuwa za kijeshi.
“Baada ya tukio, maganda yaliyookotwa yalikuwa ya
bunduki za aina ya ‘shot gun na rifle’. Hata yule mfugaji aliyeuawa
bunduki yake imesalimishwa siyo ya kijeshi,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment