Mlinzi wa kituo cha mafuta cha Ten Oil kilichopo katika eneo la Changalawe kata ya Mletele katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Mkoani Ruvuma Shaban Mustafa (45) amekutwa ndani ya kisima cha mafuta
akiwa amekufa.
Habari zilizopatikana jana Mjini Songea ambazo zimethibitishwa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki zimesema kuwa
tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili asubuhi kwenye kituo hicho
cha mafuta ambacho kipo nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
Kamanda Nsimeki ameeleza zaidi kuwa Mustafa aligundulika akiwa
amefia ndani ya kisima cha mafuta na watu waliokuwa wakimtafuta baada ya
kutokuonekana tangu alipolala kwenye lindo usiku wa kuamkia juzi.
Alifafanua kuwa katika uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kuwa
kisima hicho cha mafuta kilifanyiwa usafi siku moja kabla ya tukio hilo
na inasadikiwa kuwa ndani ya kisima hicho kulibakiwa na mafuta kidogo
ambayo inadaiwa Mstafa akiwa kwenye lindo aliamua kuingia ndani ya
kisima hicho kuyachota kwa kutumia ndoo ambayo ilikutwa juu kisima na
kandambili.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo Mstafa akiwa ndani ya kisima
alikosa hewa na kumsababishia kifo ambapo inadaiwa siku hiyo kwenye
lindo alipangwa yeye na mlinzi mwingine wa kike ambaye jina lake
limehifadhiwa kwa Upelelezi zaidi.
Alieleza zaidi kuwa Mstafa baada ya kuona kisima hicho kimefanyiwa
usafi na ndani ya kisima hicho kina masalia ya mafuta alimshawishi
mlinzi mwenzake ambaye jina lake limehifadhiwa kuwa siku hiyo asifike
kazini kwa kuwa mafuta yote yameondolewa kwenye kisima hivyo mlinzi
mwenzake asifike akiwa na lengo la kutaka kwenda kuyaiba mafuta
yaliyosalia kwenye kisima.
Aliongeza kuwa mlinzi huyo wa kike baada ya kuambiwa na Mstafa kuwa
asifike alirudi nyumbani na juzi asubuhi alifika kwenye Kituo hicho cha
mafuta ili ampokee mlinzi mwenzake aliyelala lindoni lakini hawakuweza
kumkuta jambo ambalo lilimlazimu kuanza kuzunguka katika eneo la Kituo
cha Mafuta na alipofika kwenye kisima ambacho kilikuwa wazi tangu
kiliposafishwa ghafla aliiona ndoo pamoja na kandambili na aliposogea
kuangalia ndani ya kisima aliona kama kuna dalili ya mtu akiwa
amelalala.
Alibainisha zaidi kuwa baada ya kugundua hali hiyo aliwasiliana na
uongozi wa kituo cha mafuta ambao ulifanya jitihada ya kuwatafuta
viongozi wa Mtaa kuwajulisha juu ya tukio hilo na baadae taarifa
ilipelekwa Kituo kikuu cha Polisi na askari Polisi mara moja wakiwa
wameongozanana na askari Polisi Mganga walifika kwenye eneno la tukio na
jitihada zilianza kufanywa za kumuokoa mtu aliekuwa ndani ya kisima
ambapo ndipo ilipogundulika kuwa ni Mstafa ambaye alikuwa ameshakufa
kutokana na kukosa hewa ndani ya kisima.
Alisema kuwa baada ya kumuopoa na kubaini kuwa Mstafa
ameshakufa mwili wake ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia
maiti ukisubiri ndugu wa marehemu kuuchukua na Polisi inaendelea kufanya
upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment