Kikosi cha wanajeshi wa Uganda ndicho kikubwa zaidi nchini Somalia
Serikali ya Uganda imewafuta kazi kwa muda wanajeshi 20 wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa nchini Somalia.

Wanajeshi hao wako nchini Somalia kupambana na wapiganaji wa kiisilamu kama sehemu ya juhudi za pamoja za AU kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab.

Msemaji wa jeshi ameambia BBC kuwa wanajeshi hao waliuza kimagendo mafuta na chakula vilivyopaswa kutumiwa na wanajeshi.

Kiongozi wa jeshi hilo Brigedia Michael Ondoga ni miongoni mwa wanaochunguzwa.

Uganda ndiyo imechangia kikosi kikubwa zaidi cha wanajeshi kwa Muungano wa Afrika wakiwa 18,000.

Kikosi hicho kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Muungano wa Ulaya kinapambana na wapiganaji wa al-Shabaab nchini Somalia.

Hata hivyo Brigedia Ondoga hajatamka lolote kuhusiana na madai hayo.

Mlo mmoja tu

Ondoga alikuwa miongoni mwa wanajeshi walioamrishwa na Muungano wa Afrika kurejea kutoka kwenye vita hivyo baada ya kudaiwa kuhusika na vitendo visivyokubalika.
 
Msemaji wa jeshi, Paddy Ankunda aliambia BBC kuwa wanjeshi 20 wataachishwa kazi kwa muda wakati matokeo ya uchunguzi yakisubiriwa.

Uchunguzi unakuja kutokana na malalamiko ya wanajeshi wa ngazi za chini waliosema kuwa wakuu wao walikuwa wanajihusisha na vitendo visivyofaa.

Madai dhidi yao yanahusu kutowalipa wanajeshi wa ngazi za chini na kuwa chakula chao kilikuwa kinauzwa.

Maafisa hao walioachishwa kazi watashtakiwa katika mahakama ya kijeshi na ikiwa watapatikana na hatia huenda wakaondolewa jeshini.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top