HATUA ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupuuza agizo la Rais
Jakaya Kikwete la kusitisha tozo la sh 1,000 kwa laini za simu (simu
card), limeiweka serikali katika wakati mgumu, huku wabunge wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wakishutumiwa kwa kuwadanganya Watanzania.
Hali hiyo imetokana na hatua ya TRA kuziagiza kampuni za simu
kuhakikisha kuwa zinaanza kutoza kodi ya laini za simu kwa miezi mitatu
tangu Julai hadi Septemba, kwa wananchi wote wanaomiliki laini za
simu.
Barua hiyo iliyosainiwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, Harry
Kitilya, Septemba 12, mwaka huu kwenda kwa wakurugenzi wa Vodacom,
Airtel, MIC Tanzania Ltd, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania na Dovetel
Tanzania inazitaka kampuni hizo zilipe tozo hiyo.
“Sheria ya fedha ya mwaka 2013 ilianzisha kodi ya laini za simu na
gharama za kutuma na kupokea pesa, tarehe ya utekelezaji ilipaswa
kuanza Julai 1, mwaka huu… tumepitia kumbukumbu za makusanyo yetu
kupitia sheria hiyo mpya ya fedha ya mwaka 2013, tunasikitika kuwa
malipo haya hayakufanyika, tunahitaji malipo hayo yafanyike ndani ya
siku 14,” ilisema barua hiyo.
Hata hivyo katika barua yao ya Julai 5, kwenda kwa Kitilya, Umoja wa
Kampuni hizo (MOAT), umeeleza kushangazwa kwao na hatua hiyo ya TRA,
huku ukitambua kuwa agizo hilo limesitishwa na linafanyiwa uchambuzi.
Aidha, kampuni hizo zimekiri kuwa hatua ya kuwataka kuwakata tozo
wateja wao ni mbaya na itaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.
“Tunaelewa kuwa lengo la tozo hii ni kuongeza mapato, lakini
kampuni za simu zimesajiliwa na zinalipa kodi kupitia TIN ya kila
kampuni, njia hii ya kutoza kodi laini za simu itaongeza ugumu katika
serikali kufikia malengo yake,” kampuni hizo zilisema.
Zilisema hata huduma iliyokuwa inatamkwa na serikali haikupewa
ufafanuzi wa kutosha, kwani kampuni za simu ziliweka bayana kuwa huduma
ya kuweka pesa ilikuwa haitozwi kodi, hivyo serikali ilipaswa
kufafanua wanapotaja huduma za simu walimaanisha huduma zipi, jambo
ambalo serikali haikufanya hadi TRA walipodai kuanza malipo hayo.
Hatua ya TRA imepokewa kwa hisia tofauti na Watanzania wa kada
mbalimbali, huku lawama zikisukumwa kwa wabunge wa CCM kwa kutumia
mbinu za ‘funika kombe’ baada ya kuona hoja ya Mbunge wa CHADEMA,
Halima Mdee, ingezua balaa bungeni.
Kuzuka kwa mjadala huo mzito ulimsukuma Rais Jakaya Kikwete kuagiza
serikali kukutana na kampuni za simu kuangalia namna ya kushughulikia
jambo hilo, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye, akijigamba kuwa serikali ya CCM ni sikivu, na kwamba suala hilo
halitatekelezeka.
Uamuzi huu mpya wa TRA ni uthibitisho kuwa kauli za Rais Jakaya
Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi wengine wa CCM
zinaonekana kama zilizokuwa na lengo la kupunguza jazba za wananchi na
wadau mbalimbali waliopaza sauti zao kupinga tozo hiyo muda mfupi baada
ya Bunge la mwezi Julai.
Wachambuzi wa siasa wanasema CCM walifahamu mapema tozo hiyo ni mwiba
kwao, siku ya kusomwa kwa bajeti kuu ya serikali, Waziri wa Fedha na
Uchumi, William Mgimwa, alilazimika kufuta pendekezo la awali katika
kifungu (C ) (viii) cha marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa, sura
147, akisema kimefanyiwa marekebisho.
Katika kikao cha Bunge la Bajeti, wabunge wengi walizima hoja binafsi
ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambayo pamoja na mambo mengine
ilisema:
“Jambo la kusikitisha ni kwamba, kipengele kilichokuwa
kinapendekeza kodi ya shilingi 1,450 kwa kila laini ya simu, ambacho
Waziri wa Fedha alilitangazia Bunge kwamba kimefutwa kilirejeshwa
kinyemela (ila kikiwa na pendekezo la shilingi 1,000), na kwa kuwa
wabunge walishatangaziwa na waziri wa fedha kuwa kipengele hicho
kimefutwa, walipiga kura ya ndiyo kupitisha sheria hiyo bila kujua
kwamba kipengele kile kilirudishwa kinyemela.
Kwa mujibu wa Mdee, tukio hilo lilidhihirisha kwamba serikali
ililihadaa na kulidanganya Bunge, hivyo kufanya maamuzi yasiyo sahihi,
na viongozi wa CCM walihadaa wananchi kwa majibu mbalimbali nje ya
Bunge.
Mbali na tozo hiyo kwenye laini za simu, serikali pia inatoza ushuru
wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote za simu za kiganjani
badala ya muda wa maongezi.
Suala ambalo wananchi wengi hawajagundua ni kodi ya zuio ya asilimia
10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mikononi,
yaani M-Pesa, Tigo-Pesa, Aitel Money na Easy Pesa.
Licha ya Waziri Mgimwa kusema ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa
kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha, tayari makali hayo
yameshaanza kuwasulubu watumiaji wa simu tangu Julai, kwani kampuni
hizo zimeongeza tozo kwenye huduma hizo za kutuma na kupokea fedha.
Wakati Nape akisema kuwa CCM inataka serikali ifute kodi hiyo kwa
madai kuwa ni mzigo kwa walalahoi, Pinda alidai fedha hizo
zitakazokusanywa zilipangwa kuingizwa REA ili kusambaza umeme vijijini.
Kauli ya Pinda inakinzana na maelezo ya Waziri wa Fedha bungeni,
ambapo alisema kuwa fedha zitakazopelekwa REA ni zile za tozo mpya ya
mafuta ya petroli (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita, ambayo
itakusanywa na TRA.
0 comments:
Post a Comment