WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi amekwepa mdahalo wa ‘Bunge tulitakalo dhidi ya muswada wa
sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013’, ambao ungemkutanisha na
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, leo mchana katika
ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mdahalo huo umeandaliwa na asasi ya kiraia ya kufuatilia mwenendo wa
Bunge na utafanyika kuanzia saa saba mchana hadi saa 12:00 jioni.
Licha ya waandaaji wa mdahalo huo kuthibitisha kumwalika Lukuvi ambaye
pia ni Mnadhimu wa Serikali Bungeni, waziri huyo amekataa katakata
kupokea mwaliko huo akisema hakuna taarifa yoyote ofisini kwake kuhusu
mdahalo huo.
“Nilikuwa katika ziara mikoani, nimekuja ofisini jana sikupata mwaliko
wowote ofisini, nimesoma katika gazeti lako na huenda gazeti lenu
likawa sehemu ya walioandaa mdahalo ndiyo maana mkawa na taarifa.
“Ninakwenda Iringa kuendelea na kazi nyingine, kwa kuwa sina taarifa za mdahalo, hivyo sitakuwapo,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa asasi iliyoandaa mdahalo huo, Marcus Albany, alilithibitishia Tanzania Daima kuwa Lukuvi alialikwa.
“Kongamano hili liliandaliwa lifanyike tangu Agosti mwaka huu,
tuliwapa barua washiriki wote, msaidizi wa ofisi ya Lukuvi ndiye
alituomba tuahirishe kwa sababu waziri huyo asingekuwapo ofisini.
“Tulipoliandaa tena mara hii barua imepelekwa ofisini kwa Lukuvi tangu
Septemba 23. Nami nilimpigia simu mara mbili hakupokea, nikatuma ujumbe
mfupi nikitaja majina yangu mawili, cheo changu na taasisi ninayofanyia
kazi na kueleza sababu za kumtafuta lakini hakutoa majibu mpaka leo,”
alisema.
Akifafanua juu ya mdahalo huo, Albany alisema umewekwa ili
kuikutanisha mihimili ya Bunge na Serikali kusudi wananchi waweze
kubaini nini hasa kinachobishaniwa katika muswada huo.
“Kumekuwapo na mvutano, kumekuwapo na sintofahamu, kule bungeni
wabunge wanabanwa na kanuni, akilazimishwa kukaa anatii mamlaka ya kiti.
“Hapa tunataka tuwape uwanja mpana ili kila upande usikilizwe vya
kutosha na wananchi, kwa kuwa suala la Katiba ni suala la wananchi,
wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo tunataka tuje tujadili tuone
wapi tumekosea na nini kifanyike kwa masilahi ya nchi,” alisema.
Albany alisema wazungumzaji wakuu katika mdahalo huo watakuwa ni Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na Lukuvi, ambaye
ushiriki wake unatiliwa shaka kutokana na msimamo alioueleza jana.
Waalikwa wengine ni Prof. Rose Mushi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba na wabunge wote wa
mkoa huu, japokuwa hadi jana wabunge wa CCM walikuwa hawajathibitisha
ushiriki wao.
Albany alibainisha kuwa katika mdahalo huo asasi mbalimbali za kiraia,
vyama vya siasa, taasisi za elimu ya juu nchini, viongozi mbalimbali wa
dini na wadau wanaopenda kuchangia mawazo yao kuhusu muswada huo
wanaalikwa.
Tangu kupitishwa kibabe kwa muswada huo wenye kasoro nyingi, vyama
vitatu vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi vimeunganisha nguvu
vikizunguka sehemu mbalimbali nchini kushawishi makundi mbalimbali na
wananchi wamshinikize Rais Jakaya Kikwete asiusaini.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment