Kukithiri kwa rushwa miongoni mwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi nchini, kumesababisha silaha ndogondogo hususan bastola kumilikiwa na watu wasio na sifa nchini.
 
Uchunguzi wa kina wa gazeti hili katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo iliyopo mipakani inaonyesha kuwa, bastola zinamilikiwa na watu bila ya kufuata taratibu na nyingine zikitumika kwa ajili ya kufanyia uhalifu.
Hivi sasa hata vibaka ambao awali walikuwa wakitumia visu na mbao za misumari kupora mali za watu, sasa wanafanya uhalifu huo kwa kutumia bastola.
Mbali ya vibaka kumiliki bastola, wahamiaji haramu walioko ndani ya mipaka ya Tanzania inayopakana na Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanadaiwa kuingiza silaha nzito, ambazo zinatumika kwa ajili ya matukio ya kihalifu.

Jinsi silaha zinavyopatikana
Uchunguzi unaonyesha moja ya njia ambayo imekuwa ikitumika watu wasiokuwa na sifa kupata bastola au bunduki ni kutumia mawakala au baadhi ya maofisa polisi, waliopo katika mikoa mbalimbali ambao huwatafutia vibali vya kumiliki.
Utaratibu wa kawaida ni kwamba waombaji wanaotaka kumiliki silaha ni lazima wajadiliwe katika kamati za ulinzi na usalama za mtaa au kijiji, wilaya na mkoa na kuhojiwa ili kujiridhisha kama mwombaji ana sifa.
Mkoa wa Kilimanjaro
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya vijana wadogo wakiwamo wafanyabiashara, wana vibali vya kumiliki bastola mkoani Kilimanjaro na hawakupitia mchakato huo.
“Unataka kibali cha kumiliki bastola? Una milioni moja na nusu nikuunganishe na jamaa Dar anakufanyia process (mchakato) zote anakuletea kitabu,”alisema kijana mmoja jina tunalihifadhi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi makao makuu na wale waliopo mikoani, wamegeuza suala la kumilikisha watu silaha kama mradi wa kujitajirisha.
“Tatizo la nchi hii ni corruption (rushwa) kwa sababu unajiuliza hivi hawa vijana wadogo kabisa wanamiliki bastola na hawakujadiliwa kwenye kikao chochote,”alidokeza mfanyabiashara mmoja.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wapo wanaojiita wafanyabiashara, lakini ni matapeli wa kimataifa nao wamepewa vibali vya kumiliki bastola na wakati mwingine huzionyesha waziwazi wakiwa baa.
“Ufyatuaji wa risasi siku hizi umekuwa holela…ninavyofahamu ukifyatua hata risasi moja, lazima uandikishe maelezo polisi ulifyatua kwa sababu zipi siku hizi lakini hilo halifanyiki,” ilidokezwa.
Inadaiwa kuwa kutokana na kuwapo kwa ulegevu wa vyombo vya dola hususan Polisi, baadhi ya wamiliki wa bastola hizo wamekuwa wakizikodisha kwa majambazi ambao huzitumia katika uporaji.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ulegevu huo katika kudhibiti matumizi ya silaha, kumetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki kukodisha bastola zao na kurudishiwa baada ya matukio pasipo kugunduliwa.
Dar es Salaam
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria jijini Dar es Salaam, kumeongeza matukio ya uhalifu.
Baadhi ya watu ambao wapo karibu na maofisa wa polisi makao makuu wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwatafutia watu vibali vya kumiliki silaha.
Watu hao wamekuwa wakijipatia Sh600,000 hadi Sh900,000 kwa kibali kimoja cha kumiliki silaha.
Hali hiyo imesababisha wahalifu wengi wakiwamo vibaka mitaani kumiliki silaha ambazo wanazitumia kupora watu mitaani.
Mussa Radhamn Mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam anasema hali ni mbaya, hivi sasa hata vijana wasiokuwa na kazi wanamiliki silaha.
Alisema hivi sasa huwezi kupita uchochoroni kuanzia saa 4:00 usiku, lazima utakutana na vibaka wakiwa na bastola.
Wahamiaji haramu
Mkoa wa Kagera
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Ngara alisema kuwa silaha nyingi hasa bunduki za rashasha (sub machine gun) zinanunuliwa nchini Burundi.
“Wakati kambi za wakimbizi za Lukole zikifanya kazi, silaha zilikuwa zikipatikana kwa wingi, lakini kwa sasa kwa kuwa wakimbizi hao wameondoka, silaha zinafuatwa hukohuko,” alisema na kuongeza:
“Kuna watu wana uhusiano na wenyeji wa Burundi, basi wanaziagiza tu… bunduki moja ya SMG ni kama Sh200,000 wanakuletea. Unajua kule kwa sasa kuna njaa kali kwa hiyo yale makundi ya waasi yalikuwa na silaha nyingi hayana jinsi ila kuziuza ili kujikimu kimaisha.”
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Uhamiaji katika mpaka wa Rwanda na Tanzania (Rusumo), Mahirande Samuel alisema ni vigumu kudhibiti wahamiaji haramu hasa katika mpaka wa Burundi kwani ni mkubwa na uwezo ni mdogo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alisema wahamiaji hao wamekuwa wakishiriki katika matukio ya uhalifu wakishirikiana na wenyeji.
“Wahamiaji haramu wamechangia sana katika matukio ya uhalifu. Wanaharibu mazingira kwa kuchoma misitu, kuchoma mkaa, kupasua mbao na ujangili. Tunafaya juhudi kutekeleza agizo la Rais la kuwaondoa nchini na kazi inaendelea vizuri,” alisema na kuongeza:
“Hadi sasa tumeshakamata silaha aina ya bunduki za gobori 50 ambazo zimesalimishwa, ila wanaosalimisha hatuwajui maana huzitupia kwa viongozi wa vijiji na kukimbia. Silaha tulizokamata ni mbili ambazo ni SMG ikiwa na risasi 70 na gobori moja.
Akizungumzia tukio la Juni 15, mwaka huu, ambapo mabasi mawili yalitekwa na majambazi na kuwapora abiria katika pori la Kasindaga, Kamana Kalangi alisema bado uchunguzi unafanyika, lakini kuna kuhusika kwa wahamiaji haramu wakishirikiana na wenyeji.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Fabian Massawe alisema kuwa majeshi ya Tanzania kwa sasa yanajipanga kwa ajili ya operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu mkoani humo.
Kwa sasa majeshi yetu yanajipanga kwa ajili ya operesheni, alisema na kuongeza:
Kama Serikali itasaidia tunataka operesheni hii iwe endelevu, ila hatuwezi kuweka kambi za jeshi mipakani kwa sababu sheria za kimataifa haziruhusu. Operesheni hii ni kwa wahamiaji wa nchi zote zinazotuzunguka. Nashangaa Rwanda peke yao wanalalamika.

Mkoa wa Mwanza
Uchunguzi unaonyesha kuwa watu wengi wamepata silaha kwa njia ya haramu.
Baadhi ya watu wamenunua kutoka kwa wakimbizi na wengine wakipata vibali vya kumiliki kupitia kwa mawakala au maofisa wa polisi wasiokuwa waaminifu.
Lugwecha Makune Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, alisema kuwa hali ya uhalifu mjini Mwanza hivi sasa inatisha.
Alisema kuwa hivi sasa wahalifu wengi wanatumia bastola kupora watu mitaani tofauti na zamani walikuwa wakitumia mapanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo alisema yupo nje ya ofisi atalitolea ufafanuzi baadaye.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la kuwarudisha makwao wahamiaji hao, huku idadi yao ikifikia zaidi ya 10,000 waliorudi kati ya 50,000 wanaokadiriwa kuwepo nchini.
Wiki hii Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema operesheni ya kuwandoa kwa nguvu wahamiaji waliobaki itakuwa ya kushtukiza.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema atafutwe baadaye.
Hata hivyo, alipopigiwa simu alisema afuatwe ofisini kwake kulizungumzia, lakini alipofuatwa alisema alikuwa na kazi nyingi.
Maoni ya watu mbalimbali
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humprey Moshi alisema kuongezeka kwa matukio ya watu wanaotumia silaha, ni matokeo ya ukosefu wa amani katika nchi za jirani ambao umesababisha wahalifu kuingia nchini kwa njia za kificho wakiwa na silaha.

Moshi anasema ukiritimba katika upatikanaji silaha serikalini si sababu ya watu kununua silaha kwa njia za siri, bali ukosefu wa ajira kwa vijana na mmomonyoko wa maadili ndivyo vilivyoifikisha hali ya kutokuwa na usalama mahali ilipo leo.
“Taratibu za upatikanaji wa silaha serikalini siyo tatizo, migogoro katika nchi jirani ndiyo inayofanya silaha zipatikane kwenye mipaka yetu,” anasema.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema suala la upatikanaji silaha haramu si la Tanzania peke yake, nchi inapaswa kushirikiana na nchi zote na kushauri serikali za mitaa kushirikiana na vyama vya siasa kudhibiti tatizo hilo.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema upatikanaji wa silaha kiholela unatokana na kubadilika kwa mfumo wa maisha na kwamba baadhi ya watu siku hizi wanamiliki silaha kama njia mojawapo ya kujipatia fedha kwa njia za uhalifu.
“Kuna mianya mingi ya kumiliki silaha kinyume na sheria, Serikali imeweka sheria ambazo ni lazima zifuatwe,” alisema.
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top