MKOA wa Katavi umeanza mchakato wa kuomba maadhimisho ya siku ya Mazingira dunia mwaka 2014 zifanyikie mkoani humo ili kupata wigo wa kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi wa mkoa huo

Hayo yalibainika katika kikao cha mkuu wa mkoa wa Katavi Dr Rajabu Rutengwe na wanahabari kilichofanyika katika ofisi yake mwishoni mwa wiki kikao kilichokuwa kikilenga kuwashukuru wananchi wa mkoa huo na wana habari namna walivyofanikisha mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani kwake

Alisema katika mkoa wake kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu hasa ufugaji holela na uingizaji mifugo kiholela unaoendelea katika mipaka ya mkoa huo na
kusababisha kupotea kwa uoto wa asili katika mmisitu mbalimbali ya mkoa huo

“Mtakubaliana name kuwa hakuna mkoa wenye uoto wa asili na misitu minene katika nchi yetu zaidi ya hapa Katavi, tuna mashaka mandhari ya Katavi itatoweka mapema kama hatujachukua hatua kwani uingizaji mifugo kiholela imekuwa na utamaduni na watu wengine wanaona kuvamia misitu kwa shughuli za kilimo ni haki yao” alisema mkuu wa mkoa

Alifafanua kuwa ofisi yake inapochukua hatua baadhi ya wafugaji wanahisi kuonewa badala ya kuangalia namna wanavyoathiri mazingira na kuharibu uoto wa asili kwani wafugaji wote walioingia mkoani humo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita waliingia kinyemela na kupata uhalali kwa njia ya udanganyifu

Alisema hivi sasa ofisi yake imeanzisha program maalumu ya kuhakikisha inazuia uingiaji holela wa mifugo na kuanza kuwachukulia hatua viongozi wa vijiji, kata na vitongoji wanaowapenyeza wafugaji kwa njia zisizo halali na kuwapa hifadhi kutokana na rushwa Dr Rutengwe alisema watendaji na viongozi wa vijiji walioshiriki kuwaingiza kinyemela.

wafugaji wameshaanza kuchukuliwa hatua na hawatasita kuwashughulikia wala rushwa mkoani kwake bila kujali nafasi zao katika jamii kwani kumekuwa na mtindo wa kupokea pesa kutoka kwa wafugaji na kuingiza
mifugo kinyemela  katika maeneo mbali mbali mkoani humo na kusababisha uharibifu wa mazingira

Akizungumzia suala la elimu ya mazingira mkuu wa Mkoa alisema mpango huo unaendelea na hivi sasa mkoa unajiandaa kuomba maadhimisho ya siku ya mazingira duniani mwaka 2014 zifanyikie katika mkoa wake

“Tunaomba ofisi ya Makamu wa Rais baada ya kuandaa mkoa wa Rukwa, maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwakani tuandae sisi hapa mkoani Kwetu ili kuweza kupata uwanja mpana zaidi wa kutoa elimu na hamasa ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wetu” alisema Dr Rutengwe

Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwaka huu 2013 yalifanyikia katika mji wa Namanyere wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ambapo mgeni rasmi alikuwa makamu wa Rais Dr Mohammed Gharib Bilal
Via Sumiablog
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top