Pichani ni baadhi ya taswira wakati wa mhadhara alipokuwa Sheikh Ponda mkoani Morogoro.

Habari zilizotufikia kutoka mkoani Morogoro zinadai kuwa Sheikh Ponda amejeruhiwa kwa risasi akiwa kwenye mhadhara mkoani humo.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile hivi punde kupitia Radio One, amesema  kuwa mpaka sasa hajapata taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo la kujeruhiwa Sheikh Ponda na bado wanaendelea na uchunguzi kupata ukweli wa suala hilo.

HAPA CHINI KUNA USHUHUDA WA MDAU ALIYEKUWA ENEO LA TUKIO KAMA ALIVYOUANDIKA KATIKA MTANDAO WA JAMII FORUM:

Kweli nimeshindwa kuamini kilichotokea, Sheikh Ponda kupigwa risasi. Nilikuwepo pale uwanjani tena nilikuja mapema kabisa na hivyo kushuhudia kila kitu kilichotokea.

Kimsingi sikuona sababu ya Sheikh Ponda kutokewa na tukio baya kiasi kile ambacho hakionyeshi ubinaadamu kabisa, utu wetu, uhuru wetu na hata heshima tuliyonayo Watanzania kwenye jumuiya za kimataifa. Mpaka sasa haieleweki ni nani hasa kampiga risasi Sheikh Ponda, lakini minong'ono ya watu wanasema ni polisi wamehusika. Binafsi pamoja na kufuatilia kwa ukaribu sikuona ilikotokea risasi hata aliyepiga na nilikuwa mbali kidogo na tukio. Ila nilimwona wakati anapandishwa kwenye pikipiki akiwa tayari amekwisha kupigwa risasi. Imewahuzunisha wengi!

Jamaa ameongea kwa muda mfupi sana ni takribani dakika 18, kwani alianza kuongea saa 11:54 na alimaliza kuongea saa 12:12 jioni. Hali ya uwanjani kwa kweli ilikuwa shwari sana, hata polisi hawakuonekana jirani walikuwa kwa nyuma kabisa huku wakiwa wamejisheheni kwa zana zote za kazi.

Mara baada ya Ponda kukaribia kumaliza kuongea alisema kuwa muda hautoshi isipokuwa alitangaza kuwa kesho baada ya swala ya adhuhuri atakuwa kwenye msikiti wa mkoa wa Morogoro wa Boma Road ambapo ataongea kwa kirefu hivyo kuwataka Waislamu kesho kuhudhuria eneo hilo.

Inavyooneka polisi walipanga wamkamate hata kabla ya kuongea katika ule mkutano na ndiyo maana walitega sehemu kana kwamba walikuwa wakimsubiri aingie wamkate. Lakini katika hali isiyotarajiwa na wengi, Sheikh Ponda iliingia uwanjani kupitia upande wa pili ambapo msafara wake ulikuwa na gari moja tu na taksi mbayambaya kiasi kwamba wala huwezi kudhania. Mara tunashangaa gari imesimaa na Sheikh Ponda na Amiri wa Wahadhiri Tanzania Sheikh Kondo Bungo wakashuka, wakapita kwenye kundi la Waislam kwa nyuma ghafla kivumo cha shangwe na Takbir kikavuma huku umati wa Waislam waliohudhuria hapo ukiitia Allah Akbar, Allah Akbar n.k.

Wakati huo jukwaani alikuwa akiongea Sheikh Said Riko na ndiyo aliyewapokea kwa kuanzisha Takbir ambayo iliitikiwa na Waislam Allahu Akbar, Allah Akbar. Kwa sababu waliingia kwa kuchelewa ilibidi mara moja Sheikh Said Rico ampishe Sheikh Kondo Bungo, Amiri wa wahadhiri Tanzania aongee. Wakati anaendelea kuongea kabla hata hajamaliza umeme ukakatika, likachukuliwa jenereta ambalo lilikuwa jirani likawashwa, na mhadhara ukaendelea kama kawaida. Sheikh Kondo Bungo akamaliza mada yake, akarudi Sheikh Said Riko, akaongea na kuchangisha michango kwa ajili ya kuendeleza harakati kwa muda wa kama dakika tano hivi ndipo akaruhusiwa Sheikh Ponda kupanda jukwaani.

Sheikh Ponda mara baada ya kumaliza kuongea, watu wakaanza kutawanyika, lkn ghafla mwendesha shughuli akatangaza waislam wasitawanyike kwanza kwa kuwa kulikuwa na matangazo.Wakati matangazo yanendelea ambayo sikuweza kuyasikia , ghafla tukaona defenda moja ya polisi inaingia ambayo ilikuwa imejaza polisi walio tayari kwa mapambano. Waislam wakawa wanawashanga kulikoni tena ilhali mkutano ulifanyika na kuisha kwa amani kabisa.

Basi Sheikh Ponda akaingizwa kwenye taxi iliyokuja kumfuata akiambatana na Sheikh Kondo Bonge. Polisi walitaka kumkamata Sheikh Ponda lakini waumini wakamkinga kwa kulizingira gari alilopanda huku likiondoka taratibu. Huku nyuma gari la polisi likawa linafuata taratibu bila kupiga risasi hewani wala kupiga mabomu ya machozi. 

Gari ya polisi ilipofika barabara ya lami maeneo ya karibu na jengo la Fire ilionekana kusimama kwa muda huko gari iliyombeba Sheikh Ponda kukunja kushoto kuelekes kwenye msikiti wa Mungu mmoja dini moja. Kabla msafara wa Ponda haujafika kokote gari nne za polisi zilikuja kwa kasi sana na kuanza kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya waumini, watu walitawanyika na Sheikh Ponda akashuka na kuelekea kwenye gereji moja hivi kabla ya kufika idara ya maji ambako ndiko alikopigwa risasi.

Kwa kweli sijui ilikotokea risasi iliyompiga Ponda, nadhani kamanda wa polisi atalitolea ufafanuzi zaidi. Mimi nimeandika kile nilichoona kwa macho yangu!

Mi nilidhani ingekuwa busara kwa jeshi la polisi kama walimuhitaji Sheikh Ponda wangemwambia anahitajika polisi na hivyo ajisalimishe.
GPL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top