ZIARA ya Rais wa Marekani, Barack Obama hapa nchini, ‘imeivua
nguo’ Serikali ya Tanzania, baada ya vyombo vya habari vya kimataifa
kutoa tuhuma nzito za vitendo vya kikatili vinavyodaiwa kufanywa na
vyombo vya dola dhidi ya raia.
Hatua hiyo inayodaiwa kujaribu kufichwa kwa nguvu kubwa na baadhi ya
watendaji wa serikali, imekuja kufuatia baadhi ya vyombo vya habari
mashuhuri nchini Marekani, kuibua upya tuhuma za utekaji, upigaji na
uuaji wa raia, waandishi wa habari na wanaharakati nchini Tanzania.
Moja ya chombo kilichoanika uovu huo, ni gazeti kongwe na mashuhuri
linaloheshimika sio tu Marekani, bali na mataifa makubwa la New York
Times, ambalo Julai 1, 2013, lilichapisha habari isemayo ‘Matukio ya
udhalimu yaongezeka Tanzania, Kisiwa cha Amani Afrika’.
Habari hizo zilizoandikwa na mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi
duniani, Nicholas Kulish zimeeleza tukio la kusikitisha la kutekwa
nyara na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini,
Dk. Stephen Ulimboka, kama moja ya tukio baya ambalo linadaiwa kuwa na
mkono wa serikali, ingawa Rais Jakaya Kikwete aliwahi kukanusha madai
hayo.
Mwandishi huyo ameeleza namna Dk. Ulimboka alivyotekwa na kupakiwa
kwa nguvu katika gari linaloaminika kuwa la moja ya vyombo vya usalama,
kupigwa kwa kikatili kwa nyaya, kung’olewa kucha, na jinsi watesaji
walivyoshauriana njia ya kumuua ikiwemo kumkanyaga na gari ama sindano
ya sumu.
Mwandishi huyo, amemnukuu, Dk. Ulimboka akisema namna alivyowasikia
watesaji wake, wakimwambia kuwa ‘atalipa yote aliyotenda’ na kumtaka
asali na kumwomba Mungu wake, kwa sababu hataiona dunia tena.
Aidha, gazeti hilo limeieleza dunia kutekwa kwa waandishi wa habari
na kuuawa kikatili kwa mwandishi wa habari, Daud Mwangosi aliyeuawa na
askari polisi akiwa kazini, katika Kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa,
mwaka jana.
Katika kuonesha uzito wa tuhuma hizo na namna wananchi wa Marekani
wanavyotaka lishughulikiwe haraka, moja ya taasisi kubwa inayotetea
waandishi wa habari duniani, yenye makazi yake jijini New York,
ilimwomba Rais Obama kumkabili Rais Kikwete watakapokutana katika ziara
yake iliyomalizika jana, juu ya matukio hayo na uhuru wa vyombo vya
habari.
Kadhalika, gazeti hilo limeanika matukio mawili ya mashambulizi ya
mabomu yaliyofanywa jijini Arusha kwenye Kanisa la Katoliki la Olositi
na katika mkutano wa chama cha upinzani, (hawakukitaja) na kusababisha
vifo vya watu saba.
Gazeti hilo pia limeeleza kwa kirefu namna shambulio la bomu la
kurushwa kwa mkono lilivyotokea katika mkutano wa CHADEMA hivi karibuni
huko jijini Arusha, na shutuma zilizotolewa na chama hicho dhidi ya
Jeshi la Polisi kuhusika na kumtorosha aliyelipua bomu hilo.
Kadhalika, limenukuu msimamo wa CHADEMA wa kukataa kukabidhi kile
kinachosemakana ‘mkanda mzima’ wa tukio hilo kwa polisi, hadi pale
itakapoundwa tume huru kuchunguza tukio hilo.
Msimamo huu wa New York Times, wa kuichimbua Tanzania na kuyaanika
maovu yake yote unaungwa mkono pia na magazeti mengi nchini Marekani,
kama vile USA Today, ambalo nalo limechapisha habari zenye msimamo kama
huo, likionesha wazi namna ziara ya Rais Obama ilivyotoa fursa
‘kumulikwa’ kikamilifu kwa matukio mabaya yaliyoikumba nchi.
Inadaiwa kwamba mara baada ya waandishi hawa wa Marekani kupata
taarifa kutoka kwa Wizara ya Nje ya Marekani (State Department), juu ya
ziara ya Obama hapa nchini, walianza kujipanga kufichua maovu
yanayotendwa na Serikali ya Kikwete.
Vyombo hivyo, vikafichua matukio mabaya yakiwemo uvunjwaji wa haki za
kibinadamu, matukio ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa upande wa
polisi, kutokamilika kwa uchunguzi kwa matukio ya kihalifu na uhasama
baina wa wafuasi wa chama tawala na wale wa upinzani.
Mbali na matukio hayo, vyombo hivyo, kinyume na vya hapa nchini ambavyo vimesifia ziara ya Obama, vimejikita kuibua uozo uliopo, likiwemo pia suala la kukithiri kwa uchafu katika Jiji la Dar es Salaam.
Chombo kingine kilichoandika mabaya ya Tanzania ni wavuti ya eTurbroNews ambayo inaandika kuhusu masuala ya utalii.
Watuti hiyo, Julai 1, 2013, iliibua habari za uchafu uliokithiri
jijini Dar es Salaam, na kulitaja kuwa mojawapo ya majiji yanayosifika
kwa uchafu likishika nafasi ya 12 duniani.
Habari hiyo imeushutumu uongozi wa jiji kwa kuamka dakika za majeruhi
kufanya usafi na kujiuliza ilikuwaje wasubiri hadi ziara ya Obama
kufanya kazi hiyo.
Aidha, habari hiyo imezungumzia kero ya kunguru weusi, na kushauri
pengine ianzishwe kampeni ya watu kutoka nje kuja kuwawinda na
kuwaangamiza kabisa, kama mchezo wa uwindaji, kwani sasa idadi ya
kunguru hao waharibifu inazidi milioni moja.
Picha kwa hisani ya mtandao
0 comments:
Post a Comment