Jaji mkuu wa mahakama ya juu zaidi ya kikatiba
ameapishwa nchini Misri kuwa rais wa muda baada ya jeshi kumng'oa
mamlakani rais aliyechaguliwa na raia kwa njia ya kidemokrasia na
kushinda kwa wingi wa kura, Mohammed Morsi.
Viongozi duniani wamepokea kwa tahadhari matukio
yanayojiri huko Misri. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Guido
Westerwelle, amewaambia waandishi kwamba anaangalia kwa umakini hatua
iliyochukuliwa na jeshi la Misri.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa
Uingereza , William Hague, amesema Uingereza haiungi mkono uvamizi huo
wa kijeshi lakini haina budi kuitambua hatua hiyo na kusogea mbele. Hata
hivyo alikataa kulishutumu jeshi kwa kumpindua Morsi akisema ni uvamizi
ulioungwa mkono na watu wengi.
Mfalme Abdalla wa Saudia ametuma ujumbe wa
hongera kwa kaimu rais wa Misri akisema kwamba uteuzi wake unajiri
katika wakati muhimu.
Mkuu wa jeshi Generali Abdul Fattah al-Sisi
alitoa tangaza hilo kupitia televisheni Jumatano jioni, katika kile
Morsi, alisema ni mapinduzi ya kijeshi.
Generali Sisi alisema kuwa Morsi, ambaye ni rais wa kwanza kuchaguliwa amekosa kutimiza mahitaji ya watu.
Hatua hiyo inakuja baada ya siku nyingi ya maandamano, dhidi ya rais Morsi wa chama cha Musolim Brotherhood.
Waandamanaji walimtuhumu yeye na chama chake kwa
kusukuma ajenda ya kiisilamu kwa taifa hilo na kukosa kusuluhisha
matatizo ya kiuchumi yanayokumba taifa hilo.
Chama cha Muslim Brotherhood kimesema kuwa bwana
Morsi pamoja na washauri wake wako chini ya kifungo cha nyumbani na
hawana mawasiliano ya nje.
Hapo awali mkuu wa majeshi alisema kuwa katiba
ya nchi hiyo imeahirishwa na kwamba jaji mkuu wa taifa hilo atachukuwa
mamlaka ya rais.
Maelfu ya waandamanaji wanaompinga bwana Morsi
mjini Cairo walisherehekea kwa shangwe na vifijo kufuatia taarifa hiyo
ya jeshi lakini wale wanaomuunga bwana Morsi wanasemekana kubaki kimya
huku wakisubiri matukio yatakayofwata.
Rais Obama amesema kuwa ana wasiwasi mkubwa
kuhusiana na matukio yaliyopo nchini Misri huku katibu mkuu wa umoja wa
mataifa Banki Moon akitaka kuwe na utulivu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment