Matumizi ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa mwaka ujao wa fedha yameiweka Serikali njia panda hasa baada ya kutakiwa kutafuta fedha hizo nje ya bajeti.

Kamati ya Bunge ya Bajeti imeweka wazi kuwa fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya shirika hilo linalotegemea zaidi ruzuku ya Serikali, ni ndogo kuliko mahitaji halisi ya Shirika hilo kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo, Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi,  Andrew Chenge  na wabunge wameungana kuitaka Serikali kutobadilisha matumizi ya fedha zilizopangwa na Bunge katika bajeti yake, huku wakiitaja Wizara ya Nishati na Madini kuwa moja ya wizara zilizotumia fedha zaidi ya bajeti waliyopangiwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa Chenge, Wizara ya Nishati na Madini katika mwaka wa fedha unaoisha, ilipangiwa kutumia Sh bilioni 76.99 lakini ikatumia Sh bilioni 148.42, sawa na ongezeko la Sh bilioni 71.43.

Wizara nyingine zilizotumia fedha zaidi ya bajeti ilizopangiwa ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo ilipangiwa kutumia Sh bilioni 80.6 lakini ilitumia Sh bilioni 112.08 sawa na ongezeko la Sh bilioni 31.47.

Pia Wizara ya Afya, lipangiwa kutumia Sh bilioni 219.36 lakini ilitumia Sh bilioni 246.71, sawa na ongezeko la Sh bilioni 27.35. Deni la Taifa nalo, lilipangiwa kutumia Sh trilioni 1.9, lakini lilitumia Sh trilioni 2.5 sawa na ongezeko la Sh bilioni 624.

Akizungumzia hali hiyo juzi bungeni, Chenge alisema katika hali ya kushangaza wizara hizo zimetumia fedha zaidi ya zilizoidhinishwa na Bunge.

Ili kukabili hali hiyo, Chenge akaitaka Serikali, itakapotaka kuongeza fedha zaidi ya zilizoidhinishwa na Bajeti, kwa maana ya kuhamisha mafungu, iwasiliane kwanza na Kamati yake.

Kuhusu Tanesco, Chenge alisema; "Ni muda mrefu sasa Shirika hili limekuwa likitumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme.

"Kamati imebaini kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha Shirika hili, hali inayosababisha kufanyika kwa uhamisho wa fedha kutoka katika maeneo mengine kwa ajili ya kupeleka Tanesco," alisema.

Ili kuzuia hali hiyo, Chenge alisema Kamati yake ilikutana na Tanesco pamoja na Wizara ili kupata taarifa za gharama halisi ya Tanesco kwa mwaka ujao wa fedha, ambao shirika hilo limetengewa Sh bilioni 273.

"Katika kikao hicho, ilibainishwa kwamba kwa mwaka 2013/14, Tanesco itaendesha mitambo kwa asilimia 78, na kwa mpango huo, Tanesco itatumia Sh trilioni 1.2," alisema Chenge na kuongeza kuwa mitambo hiyo ikiwashwa kwa asilimia 100, shirika hilo litatumia Sh trilioni 2.2.

Badala ya kujadili wapi fedha hizo zitapatikana, au kutoa nafasi ya Wizara kukutana na Kamati kutafuta fedha hizo, Chenge alitaka Serikali itafute fedha hizo sehemu nyingine bila kugusa bajeti. "Kamati inashauri kuwa fedha hiyo ipatikane bila kuathiri Bajeti ya Serikali," alisema.

 Wakati wa kuchangia bajeti hiyo, wabunge wengi pia walisimamia msimamo huo, bila kuitaja Tanesco, wakataka Serikali isibadilishe matumizi ya fedha zilizopangwa katika bajeti, na wengine kufikia hatua ya kutaka Sheria ya Bajeti, ili kuidhibiti Serikali isihamishe vifungu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top