Huku mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ukiwa unahitimishwa leo, wabunge wa CCM wameshindwa kupata mwafaka wa kusimama pamoja ili kuipitisha.
 
Wabunge hao walikutana jana jioni kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma kujadili tofauti baina yao na kuwa na msimamo wa pamoja, lakini mgawanyiko wa dhahiri ulionekana ndani ya kikao hicho baadhi wakipinga huku wengine wakiunga mkono na kuwatisha wenzao.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema wabunge wengi wa chama hicho walipinga bajeti hiyo wakiitaka Serikali kuzingatia mapendekezo ya marekebisho waliyoyatoa wakati wakichangia mjadala. Mambo makubwa mawili yaliyowagawa wabunge hao ni suala la kupandishwa kwa ushuru wa petroli na hatua ya Serikali kupunguza asilimia moja tu kwa kodi ya mshahara (PAYE).
Pia wabunge hao waliitaka Serikali itekeleze mapendekezo ya marekebisho yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama alitumia muda mwingi kuwashawishi wabunge kuikubali bajeti hiyo. Aliwaambia wabunge hao kuwa yeyote anayejiona hawezi kuunga mkono bajeti hiyo ni bora asiingie kwenye kikao cha kesho (leo).
Habari zaidi zinaeleza kuwa hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Sikonge, Tabora, Saidi Nkumba aliyesema anayepinga bajeti hiyo, siyo tu asiingie katika kikao hicho, bali atafute chama kingine.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema mbunge wa CCM atakayepinga ongezeko la kodi ya mafuta leo halitakii mema taifa.
Bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa Juni 13, mwaka huu ilipendekeza punguzo la asilimia moja la kodi hiyo, huku mafuta yakiongezwa kodi kwa asilimia mbili kwa dizeli na petroli asilimia moja.
Mbunge wa Geita, Dk Hamisi Kigwangalla ndiye pekee aliyepinga waziwazi bajeti hiyo kwa upande wa CCM wakati wa mjadala akisema haina jibu kwa suala la ajira kwa vijana, mfumuko wa bei, njaa, uhakika wa chakula na afya. Pia alipinga ongezeko la kodi.
Licha ya kuunga mkono bajeti hiyo, wabunge wengine wa CCM waliikosoa wakibainisha kasoro kadhaa. Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba alisema inawapa mzigo wafanyakazi kwa kuwapunguzia PAYE kidogo wakati kwenye simu, mafuta (petroli na dizeli), vinywaji vyote kodi imeongezwa.
Mbunge wa Kisesa, Luhanga Mpina na Kangi Lugola wa Mwibara kwa nyakati tofauti, waliikosoa wakisema inamkandamiza Mtanzania wa kawaida. 

Bajeti hiyo inayokadiriwa kufikia Sh18.2 trilioni imeelekeza nguvu zaidi katika sekta za maji, nishati ya umeme, miundombinu ya barabara, ujenzi wa bandari, reli, na elimu.
Bajeti ya mwaka huu haikujadiliwa na wabunge wa Chadema kwani hawakuwapo kwa takriban wiki nzima. Pia hakikusoma bajeti yake mbadala bungeni kutokana na wabunge wake kwenda Arusha baada ya kutokea kwa mlipuko wa bomu Juni 15, kwenye Uwanja wa Soweto wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani na kusababisha vifo vya watu wanne, kujeruhi zaidi ya 60.

Wabunge hao wanarejea bungeni leo na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema jana: “Hakubaliani na mapendekezo yote yenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.”
Kauli hiyo inapingana na ile ya Spika wa Bunge, Anne Makinda Alhamisi akiwaonya wabunge kwamba ikiwa hawataipitisha Rais atalivunja Bunge. 
 
Alitaja Kanuni ya 107 (1) na (2) ambayo hutumika kukidhi matakwa ya Ibara ya 90 (2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Rais kulivunja Bunge.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top