Rais Barak Obama
Rais Barak Obama wa Marekani, akiambatana na Mke wake Michelle, anatarajiwa kutembelea nchi za Afrika Kusini, Senegal na Tanzania kuanzia Juni 26 - Julai 3 mwaka huu.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,  Ikulu.

Katika ziara hiyo Rais Obama anatarajiwa kusisitiza juu ya nafasi ya uhusiano uliopo kati ya Marekani na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo ziara hiyo pia italenga katika kupanua wigo wa kukua kwa uchumi, uwekezaji na biashara; kuimarisha taasisi za kidemokrasia pamoja na kuwekeza katika kizazi cha viongozi wajao wa Kiafrika.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Rais Obama anatarajiwa pia kukutana na viongozi  wa serikali, wafanyabiashara, vikundi vya kiraia, hasa vijana, kwa lengo la kujadili masuala ya mahusiano kati ya nchi na nchi na hata ulimwengu kwa ujumla.
 
Ziara hii kwa nchi za Kiafrika inalenga pia katika kusisitiza juu ya mchango wa Rais Obama katika kupanua na kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na watu wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara lengo likiwa kudumisha amani na ustawi wa kikanda na Ulimwengu kwa ujumla.

Rais Obama ambaye baba yake alizaliwa Kenya, alizuru Afrika  mara moja  katika muhula wake wa kwanza, alipotembelelea Ghana mwaka 2009. 

Hii inamaanisha kuwa kwa mara nyingine Rais Obama anashindwa kutembelea Kenya ambayo hata hivyo itafarijika kumwona akitua katika nchi mojawapo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top